Rais Jakaya Kikwete amemweleza Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM), kitashinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Rais Kenyatta kwa upande wake bila kutaja CCM, alisema anaamini Watanzania wataendelea kuiunga mkono Serikali na chama ambacho kimeweza kuwaletea, amani, umoja na maendeleo.
Marais hao walitoa kauli hizo katika mji wa Taveta wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Taveta –Voi – Mwatete nchini Kenya, yenye urefu wa kilomita 98.4 kwa kiwango cha lami.
Ujenzi wa barabara hiyo unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), kwa Sh8.4 bilioni za Kenya (takriban Sh168 bilioni), ulianza Mei 2014 na utakamilika Mei 2017.
Rais Kikwete alimweleza Rais Kenyatta pamoja na wananchi wa nchi hizo mbili waliohudhuria sherehe hizo kwamba amefurahi kupata fursa ya kuwaaga Wakenya.
“Rais amenialika wakati mzuri. Baada ya siku 21 kutoka leo (jana) tutakuwa tunapiga kura kuchagua Rais mpya,” alisema na kubainisha kuwa wananchi hao walikuwa na shauku la kujua rais ajaye ni nani.
“Mnaniuliza yupi? Atatoka chama changu tu, hilo sina wasiwasi nalo na Watanzania wanajua hilo. Hii ni nafasi nzuri ya kuja kuwaaga wenzangu wa Kenya,” alisema Rais Kikwete, kauli iliyoibua makofi na vicheko.
Rais Kenyatta alimtakia kila la heri Rais Kikwete wakati anapojiandaa kuondoka madarakani akimtaka amsaidie kuonyesha njia ni kazi gani marais wastaafu wanatakiwa kufanya wanapostaafu urais.
“Sisi pia utatuonyesha barabara ni kazi gani rais mstaafu huwa anafanya wakati wetu ukifika ili tujue tunaelekea wapi. Tunakutakia kila la heri katika kampeni za uchaguzi,” alisema.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, CCM kimemsimamisha Dk John Magufuli kupeperusha akichuana zaidi na mgombea wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa na pamoja na wengine sita.
Akizungumzia miradi ya barabara inayoendelea Kenya na Tanzania, Rais Kikwete alisema barabara hizo zimefanya biashara kati ya Kenya na Tanzania kwa miaka mitano kuongezeka kwa asilimia 40. “Barabara hii ikikamilika itaongeza asimilia nyingine 10. Nimekuja tu kuwaaga, lakini nimekuja kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuwa rafiki wa Kenya,” alisema.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu hasa kwa wananchi wa mikoa ya kaskazini na kukamilika kwake kutafupisha muda wa safari hadi kufikia saa 2.30 kutoka saa 14.
Mkurugenzi wa AfDB Afrika Mashariki, Gabriel Negatu, alisema imetoa mkopo wa Dola 1.5 milioni kwa ajili ya miradi hiyo mikubwa ya barabara Kenya na Tanzania.

-mwananchi