Mfanyabiashara
maarufu nchini na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohammed Dewji
(pichani) kwa mara ya kwanza ameingia kwenye orodha ya mabilionea 29,
akiwa tajiri kijana kuliko wote barani Afrika.

Jarida la
Forbes la Marekani limemtaja Dewji (39), katika nafasi ya 24 ya matajiri
wa Afrika akiwa na utajiri wa Dola 1.3 bilioni za Marekani (Sh2.34
trilioni) unaotokana na biashara mbalimbali anazozifanya kupitia kampuni
yake ya Mohammed Enterprises (Metl Group).“Dewji alibadilisha biashara
aliyoanzisha baba yake kutoka uuzaji bidhaa na kuwa na viwanda vya
Metl,” inasema sehemu ya habari inayomuhusu bilionea huyo Mtanzania .
“Alinunua
viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei
ndogo na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa
menejimenti,” inaongeza ripoti hiyo.
Metl ina
viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu
vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4
milioni za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.
Katika
kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa
nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa
zote.
Kwa mujibu
wa tovuti yake, Metl inaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji
bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo, vinywaji na
vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji baiskeli.
Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Dewji
anashika nafasi mbili juu zaidi ya kada maarufu wa CCM na aliyekuwa
mbunge wa Jimbo la Igunga, Aziz Rostam (50) aliyewekwa nafasi ya mwisho.
Rostam
amefungana nafasi ya 26 na mabilionea wa Nigeria, Abdulsamad Rabiu na
Femi Otedola wenye utajiri wa Sh1.8 trilioni kila mmoja.
Orodha hiyo
ya 29 bora inaoongozwa na bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote akiwa na
utajiri wa Dola 15.7 bilioni za Marekani (Sh28.2 trilioni), kiwango
ambacho ni mara moja na nusu ya bajeti ya Serikali ya Tanzania ya mwaka
2014/15.
Forbes
linamtaja Rostam kuwa na utajiri wenye thamani ya Dola 1 bilioni za
Marekani (Sh1.8 trilioni), kiwango ambacho kimebaki pasi na mabadiliko
kutoka orodha ya mwaka jana. Rostam anamiliki asilimia 35 ya hisa katika
kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Vodacom
CHANZO: BBC.
0 comments