Akizungumza
katika mkutano huo kwenye Viwanja vya Mbagala-Zakhem jijini Dar es
Salaam, Bi. Mghwira aliwataka Watanzania kukipa dhamana chama hicho kwa
kuwa sera zake zitarejesha misingi imara iliyoasisiwa na wazee
walioipigania hadi ikapata uhuru.
"ACT-Wazalendo
tutarudisha misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa hili na ndiyo maana
kauli mbiu yetu ni Uhuru, Uzalendo na Uadilifu, vitu ambavyo vimepotea,"
alisema mgombea huyo wakati akinadi sera zake akirejea Ilani ya
Uchaguzi ya chama hicho.
Chama
hicho, ambacho leo kimezoa wanachama 150 kutoka CUF, kimeweka rekodi ya
pekee kwa kusimamisha wagombea ubunge 219 kati ya viti 265 vilivyopo,
kikiwa chama cha pili katika uchaguzi wa mwaka huu kilichosimamisha
wagombea wengi baada ya CCM.
Bi.
Mghwira alisema, chama chake kina watu makini na kwamba Zitto Kabwe,
ambaye ndiye kiongozi mkuu wa chama hicho, anastahili kuwa waziri mkuu
kwani juhudi zake zimeonekana katika kipindi cha miaka 10 aliyokaa
bungeni.
Awali,
Zitto akimkaribisha mgombea huyo pamoja na mgombea mwenza Hamad Mussa
Yusuph, alisema sera za chama hicho zinatekelezeka na kwamba
watahakikisha Watanzania hawapewi mzigo wa kodi unaochangia ugumu wa
maisha, kwani siri wanayo.
"Serikali
haikusanyi kodi kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa, wapo wafanyabiashara
wanaokwepa kodi kwa kuingiza bidhaa ambazo wanadai zinapelekwa nchi za
jirani wakati zinabaki hapa hapa bila kulipiwa kodi," alisema.
Alisema,
ukwepaji huo wa kodi unaikosesha serikali mapato ya Shs. 900 bilioni
kila mwaka, hivyo wao wakiingia madarakani watahakikisha kazi ya kwanza
ni kukusanya kodi hizo ili zitumike kujenga hospitali na huduma nyingine
za jamii.
Zitto
alisema kwamba, ufisadi umezidi katika serikali ya Chama cha Mapinduzi
(CCM) ambapo wiki mbili zilizopita kampuni moja ya Uswisi imepewa
mkataba wa kuingiza mafuta kwa mkupuo (bulk petrol) wakati zabuni hiyo
haikutangazwa.
"Katika
mkataba huo inaonyesha kwamba pipa moja la mafuta linauzwa kwa senti za
Dola 60 wakati kwenye soko la dunia pipa linauzwa senti za Dola 40, hii
maana yake ni kwamba watu waliopiga dili watavuna bila jasho kiasi cha
Shs. 20 bilioni huku wanaoumia wakiwa ni Watanzania wenyewe kwa kuwa bei
ya mafuta haiwezi kushuka," alisema.
Naye
mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo, aliwataka Watanzania
kuichagua ACT-Wazalendo kwa kuwa sera zake zitairudisha heshima na taifa
pamoja na misingi yake imara.
"Kuna
wengine wanafuata mbwembwe za wanasiasa walaghai, hapa sisi tunanadi
sera, kwa sababu taifa hili limepoteza misingi yake ikiwa ni pamoja na
miiko ya viongozi," alisema.
Aidha, aliibeza kauli ya Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye kwamba rais wa nchi ni meneja tu.
Sumaye
aliitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za Ukawa kwenye
Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kazi ya urais
siyo kubeba zege.
"Inashangaza
mtu aliyekaa ndani ya serikali kwa miaka mingi anathubutu kusema kwamba
kazi ya urais ni umeneja, mtu wa namna hiyo akija mkataeni mwambieni
hatutaki meneja wa miradi.
"Miaka 50
baada ya uhuru tumesomesha mameneja wengi, wahandisi wengi na kadhalika
ambao wanaweza kuifanya kazi hiyo, Rais anatakiwa awe mbunifu, siyo mtu
wa kusahau alichokisema jana. Tunataka mtu anayetoa kauli inayofanana
juzi, jana, leo na kesho wala si mtu wa kukariri," alisema Profesa
Mkumbo.
Aidha,
aliongeza kwamba rais mbali ya kuwa mbunifu, asiwe mwenye papara katika
kutoa maamuzi na alinde umoja na muungano pamoja na tunu zake.
Chanzo; habari za jamii blog
0 comments